Chama cha siasa ili kiweze kuimarika kinahitaji watu, tena watu walio imara. Na watu hawa utengenezwa kutokana na matunda ya chama chenyewe. Kazi, juhudi na maarifa ndio mwongozo wa uimarishaji wa chama cha siasa.

Ni wazi sasa baada ya kufanya utafiti wa zaidi ya miaka 5 wa katiba ipi inafaa kuwa katiba bora ya wananchi na ni ipi inaweza kuwa Itikadi yenye kuishi ndani ya watu, na sasa chama kimepata mwarobaini wake.

Katiba ya sasa ya NCCR-Mageuzi inayobeba Itikadi ya UTU ambayo misingi yake ni ya kujenga usawa, udugu, maadili, haki, Imani, mabadiliko, wajibu, asili pamoja na kazi imeonyesha kuungwa mkono kila kona nchini.

Hii leo April 23, 2020 NCCR-mageuzi imeendelea kujizolea wanachama kutoka vyama mbalimbali. Wanachama zaidi ya 70 wameamua kuitikia wimbo wa UTU kwa kukabidhiwa kadi za uanachama rasmi wa NCCR-Mageuzi, 11 kati yao ni kutoka chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) na 59 ni kutoka chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA.

Miongoni mwa majina yanoyozunguzwa haswa kati yao ni pamoja na aliyekuwa Mratibu wa baraza la Vijana (BAVICHA) Wilaya ya Morogoro 2010-2014 na kuwa Katibu mkuu kata ya Boma kupitia CHADEMA, ndg; Chage Alex Chage, pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA kata ya Boma na mratibu wa kampeni za mgombea ubunge wa CHADEMA Jimbo la Morogoro Mjini 2015, ndg; Victor Ndibalema

Zipo sababu nyingi zinazotajwa kwa wao kuweza kumtimka kwenye vyama vyao huku sababu kuu ikiwa ni matakwa ya katiba za vyama vyao. Moja ya viongozi, ndg. Victor Ndibalema yeye amenukuliwa akisema mbali na sababu nyingine nyingi lakini pia anatimiza matakwa ya katiba ya chama chao cha Chaema yam waka 2006 toleo la mwaka 2016, ibara ya 5.4 (1) inayosema mwanachama atakoma uanachama wake kwa kujiudhuru mwenyewe kwa hiyari yake, kufariki au kufukuzwa ndani ya chama.

Zoezi la kukabidhi kadi uanachama kwa wanachama wapya wanaojiunga na chama chetu cha NCCR-Mageuzi linaendelea Mkoani Moogoro. Picha na Chage Alex Chage

Sababu nyingine za kujivua uanachama wa Chadema

  1. Sababu za kujiudhuru zinatoka ibara ya kumi na tatu (13) kifungu kidogo cha kumi (10) cha katiba ya NCCR- Mageuzi, ambayo inasema kiongozi awe tayari kukubali kukosolewa pale anapokuwa na mapungufu na awe tayari kujirekebisha, kitu ambacho CHADEMA hakipo na ni makosa makubwa kumkosoa kiongozi , utaitwa msaliti au unatumika na  Chama Cha Mapinduzi (CCM).
  2. CHADEMA kuna kitu kinaitwa kamati ndogo ya kamati kuu, kitu ambacho hakitambuliki kweye katiba na kimekuwa kikifanya maamuzi kuliko kamati kuu yenye wajumbe wengi, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA. Hivyo ni vyema Mwenyekiti wa CHADEMA akawaeleza wanachama wake, anapata wapi mamlaka hayo ya kuvunja katiba?

Kwenye chama cha NCCR-Mageuzi kamati kama hizo zipo kikatiba na zinaitwa kamati maalum na haziteuliwi na Mwenyekiti bali zinachaguliwa na halmashauri kuu na hiyo ndiyo dhana nzima ya kuongoza chama kama taasisi.

  1. CHADEMA iliyokuwa inapinga kauli mbiu ya zidumu fikra za Mwenyekiti sasa imetengeneza miungu watu wake, na kwamba yeyote anayehoji mienendo ya Mwenyekiti hushambuliwa na kutengwa.
  2. Ndani ya CHADEMA ya sasa kama unataka kuwa kiongozi ni lazima ukubali kuimba mapambio ya “Mwamba tuvushe” badala ya siasa za kuunganisha wanachama na kuimarisha chama.
  3. CHADEMA iliyokuwa inapinga rushwa, uonevu na dhuluma ndio baba wa vitendo hivyo vya sasa. Ushahidi ni vitendo vilivyofanyika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu ndani ya chama na siku ya uchaguzi wenyewe, mfano hai ni uchaguzi ndani ya mkoa wa Morogoro, uchaguzi uligubikwa na vitendo vya rushwa, ulaghai na siasa za makundi.
  4. Kitendo cha kuchukuliwa fedha iliyokuwa fixed kwenye akaunti ya Ecco Bank kwa ajili ya michango ya wabunge kusaidia kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, lakini fedha hizi zimetumika nje ya utaratibu uliowekwa na chama, fedha nyingi zilichukuliwa kwenda kununua matrekta kwa ajili ya kilimo binafsi mkoani Morogoro. Kwa bahati nzuri mashamba yalikuwa ya umma serikali wakayapokonya hivyo kukisababishia chama hasara kubwa. CHADEMA kwa kukosa ama kwa kushindwa kuwa wawazi kwenye Matumizi ya fedha walifungua makampuni hewa ili kunusuru mkwapuaji huyo na kumwepusha na kashfa ya ufisadi wa fedha za michango ya wabunge, huu ni wizi na unapoteza uhalali wa kupigania haki za watanzania.

Matumizi mabaya ya fedha za chama, ukija kwenye ukurasa wa 33 ya katiba ya NCCR-Mageuzi, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi hahusiki na mambo yoyote ya fedha na wala sio signatory, pia hahusiki na mambo ya fedha za chama hivyo ukiona kuna chama cha siasa Mwenyekiti wake anakuwa mtendaji kuna uwalakini.

7. Ndani ya mkoa wa Morogoro wenye wabunge watatu wa majimbo na mmoja wa viti maalumu wameshindwa kuwa na ofisi ya chama badala yake kazi za chama kufanyika kwenye kibanda cha tigo pesa.

Wamemalizia kwa kusema kuwa,

Ikumbukwe kuwa shabaha ya chama chochote cha siasa ni kuchukua dola ili iendeshe serikali. Duniani kote hakuna shabaha ya chama cha siasa kinachopenda kuendelea kuwa chama cha upinzani. Shabaha hiyo lazima iwekwe kama kusudio au dhumuni ndani ya katiba ya chama chochote. Nasikitika kusema kuwa marekebisho “amendments” ya katiba ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya mwaka 2016 pamoja na kutoa maoni yetu ya ndani kuboresha ibara za katiba hiyo, ibara ya 4.1 hadi 4.3 (Sura ya Nne) inayohusu madhumuni ya kuanzishwa kwa chama cha siasa, chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakina dhumuni la kuchukua dola. Hii ni tofauti na mipango pamoja na mikakati ya vyama vingine.

Katiba ya CHADEMA kushindwa kutoa tamko nakushindwa kujitofautisha na taasisi za wanaharakati. Ibara ya 3.2.7 inasema kuwa CHADEMA inaamini katika siasa ambazo ziko juu ya vyama vyenye kusimamia zaidi maslahi ya Taifa. Ibara hii ndani ya CHADEMA ilishakufa. Chochote kizuri kinachofanywa na Serikali lazima kipingwe. Kuna masuala ambayo Serikali ya CCM imefanikiwa na kama Taifa tunapaswa kuwa kitu kimoja. Kuna masuala mengine Serikali ya CCM inakosea. Tunapaswa kuyapinga.

Kwanini wamechagua kujiunga na NCCR-Mageuzi?

Zipo sababu nyingi walizotaja kuwa ndio chachu ya kuchagua kujiunga na NCCR-Mageuzi kubwa ikiwa ni KATIBA yake na ITIKADI YA UTU

Wanenukuliwa wakisema kuwa, NCCR-Mageuzi ni chama kilichopitia changamoto nyingi ya kushuka na kupanda. Kimejifunza nini maana ya migogoro. Kimejifunza nini maana ya kuwa karibu na wanachama. Kimejifunza nini maana ya kukosa ruzuku. Nini maana ya kuwa na madiwani na wabunge. Historia hiyo inaifanya kuwa chama pekee Tanzania chenye uzoefu wa kufa na kufufuka kuliko vyama vyote. Chama cha NCCR-Mageuzi Kinaifanya kuwa sehemu salama kwa wana mageuzi wa kweli wanaotaka kuiondoa CCM madarakani.