Katika hali ya kuonyesha upendo wa dhati na kukubali utendaji kazi wa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Vunjo mkoa wa Kilimanjaro ndugu James Francis Mbatia, wanachama wa chama cha NCCR-Mageuzi jimboni hapo wamemtaka mbunge huyo kukubali ombi lao la kuchukua fomu ya kuwania ubunge kwenye uchaguzi wa mwezi oktoba ili aendelee kuwatumikia tena.

Zaidi ya wanachama 1,500 waliokusanyika pamoja kwa ajili ya kumtaka ndugu James Mbatia achukue fomu ya kuwania Ubunge tena, waliamua kuchangishana wenyewe fedha kwa ajili ya kumchukulia fomu ya kuwania ubunge kupitia chama cha NCCR-Mageuzi kama moja ya dhamira yao ya kumtaka aendelee kuwatumikia kwa miaka mingine tena.

Wengi wa wanachama waliopata nafasi ya kuongea kwenye mkutano huo hawakusita kutaja mambo mazuri aliyoyafanya ndugu James Francis Mbatia kwenye Jimbo la Vunjo ikiwemo matendo ya huruma anayoyaonyesha dhidi ya watu walio na kipato cha chini, wasiojiweza pamoja na watoto yatima ambao amekuwa akiwasaidia kwa fedha yake mwenyewe. Ujenzi wa miundo mbinu ya barabara na mengine mengi ambayo wananchi na wanachama wa NCCR-Mageuzi jimbo la Vunjo hawakusita kuyaweka bayana.

Kwa upande wake ndugu James Francis Mbatia ambaye ndiye mbunge wa Jimbo hilo katika bunge lililopita la 11, amekiri wazi kuwa anaheshimu mawazo ya watu wa Vunjo pamoja na heshima kubwa waliyompa na kukubali kuchukua fomu ya kuwania ubunge ili kuendelea kuwatumikia tena.

Ikumbukwe kuwa zoezi la kuchukua na kurudisha fomu ndani ya chama cha NCCR-Mageuzi limeshaanza na linatarajia kukamilika hivi punde lakini bado ndugu James Francis Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi hakuwahi kuonyesha msimamo wake juu ya kuchua au kutochukua fomu kuwania ubunge kwa miaka 5 mingine.