“Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu” Methali hii inajidhihirisha, kumezuka shutuma kubwa dhidi yetu ya kile wanachokiita usaliti. Mara baada ya kupokea viongozi wa vyama na wanachama mbalimbali kutoka katika vyama vyao na kujiunga na chama chetu cha NCCR-Mageuzi.

Hayo yote yanaibuka baada ya kuona wimbi kubwa la watu wanaimba wimbo wa UTU, UTU, UTU.

Kuhama chama kimoja na kwenda kingine si jambo geni ulimwenguni kote ikizingatia kila mmoja ana haki na uhuru wa kujiunga na chama chochote cha siasa anachokipenda. Lakini pia NCCR-Mageuzi hapo nyuma ilipoteza wanachama wengi waliohamia kwenye vyama hivyo hivyo ambavyo  leo wanatuita wasaliti na sisi hatukuwahi kulalamika.

Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara (NCCR- MAGEUZI) Ndugu Angelina John Mutahiwa akimkabidhi kadi ya Uanachama aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Ndg. Yeremia Kulwa Maganja

Akizungumza kwenye kipindi maalumu cha Medani za Siasa kinachorushwa na Televisheni ya Star TV hapa nchini mwenyekiti wa chama chetu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo ndugu James Francis Mbatia (Mb) alisema

“NCCR-Mageuzi tunashutumiwa sana na hasa viongozi na wanachama wanapohama kutoka kwenye vyama vyao kuja kwetu, mbona sisi hatukulalamika walipohamia kwenye vyama vyao? Badala yake tuliwatakiwa kila la heri, sisi leo tunahukumiwa kwa lipi?”

“Watu wanapotoka kwenye vyama vyao na kujiunga kwenye vyama vya mageuzi, tunashukuru zaidi” Alisema.

NCCR-Mageuzi ndio chama pekee sasa kinachohubiri na kuishi kwenye misingi ya UTU yenye kujali Udugu, Maadili, Haki, Usawa, Imani, mabadiliko, uhuru, wajibu, asili, kazi na endelezo.