“Viongozi uandaliwa, viongozi hawaokotwi kwenye majalala” hii ni kauli ambayo imekuwa ikisisikika mara kwa mara kutoka kwa mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, ndugu James Francis Mbatia (Mb). Dhana kuu ya kauli hii inaakisi mienendo na tabia za viongozi wengi tulio nao sasa ambao mara nyingi wamekuwa wakionesha hali ya sintofahamu katika nafasi zao za majukumu.

Ni wazi kuna sifa kadha wa kadha za kuwa kiongozi. Katiba ya NCCR-Mageuzi sura ya nne, Ibara ya 13 inaeleza wazi sifa za kuwa kiongozi, na moja ya sifa hiyo ni ile ya kifungu cha 4 ambayo inaeleza wazi kuwa kiongozi anapaswa

“Awe na upeo mpana kiakili na kuwa tayari kujiendeleza yeye binafsi kielimu na kuitumia elimu aliyoipata kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika jamii”

Kwa kuzingatia hilo Juni 27, 2020 chama cha NCCR-Mageuzi kimefanya kikao cha watia nia wake wa nafasi ya Ubunge kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu kwenye hoteli ya African Dream iliyopo mjini Dodoma. Kikao hicho kilikuwa na lengo la kutoa mafunzo kwa watia nia wote wa ubunge kupitia majimbo yote ya Tanzania bara. Jumla ya wajumbe 113 walihudhuria mafunzo hayo ikiwa wote ni watia nia wa ubunge 2020.

Wajumbe wa kikao cha watia nia wa Ubunge 2020 wakiwa kwenye mafunzo yaliyofanyika kwenye hoteli ya African Dream mjini Dodoma.

Katika kikao hicho chenye lengo la kuwanoa watia nia wa Ubunge, mambo kadha wa kadha yamejadiliwa ikiwa ni pamoja na namna ya kufanya kampeni zao kuelekea uchaguzi mkuu pamoja na mambo ya kuzingatia katika mchakato mzima wa kampeni yaani kabla na baada ya kufungwa kwa zoezi la kampeni na ile hatua ya mwisho ambayo ni ya kuhesabu kura pamoja na kutangazwa kwa mshindi.

Baadhi ya Wajumbe walipata nafasi ya kuwasilisha mada zao kwa watia nia kulingana na ujuzi na uzoefu walio nao akiwemo aliyekuwa mbunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jimbo la Moshi Vijijini ndugu Anthony Calist Komu kupitia chama cha CHADEMA ambaye amejiunga rasmi na NCCR-Mageuzi.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi ndugu James Francis Mbatia akimkabidhi kadi ya Uanachama aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Rombo kupitia CHADEMA ndugu Joseph Roman Selasini.

 

Katika kikao hicho pia NCCR-Mageuzi ilikabidhi rasmi kadi za uanachama kwa madiwani na wabunge 4 waliotangaza kujiunga na NCCR-Mageuzi siku chache zilizopita. Wabunge hao ni pamoja na wabunge wawili wa viti maalumu Bi. Joyce Bitta Sokombi pamoja na Bi. Susanne Peter Maselle.Wengine ni pamoja na naliyekuwa Mbunge w Jimbo la Rombo kupitia CHADEMA ndugu Joseph Roman Selasini pamoja na ndugu Athony Calist Komu aliyekuwa mbunge wa jimbo la Moshi Vijijini kupitia tiketi ya chama cha CHADEMA.