Jina la Mzee Maganga si geni kwenye masikio ya wanamageuzi wengi hasa unapoingia kwenye mji wenye umaarufa mkubwa kwa utengenezaji wa mafuta ya mawese, Kigoma.

Jina lake halisi ni William Maganga Kasabagi, ni askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) mstaafu lakini pia ni muasisi wa mageuzi mnamo 1993. Alizaliwa 1954. Mzee Maganga alistaafu Jeshi kwa hiari mwaka 1988 baada ya kuugua.

Harakati za Siasa

Mzee Willian Maganga alianza harakati zake za kisiasa akiwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka 39 wakati huo akiwa Mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Alijiunga na chama cha NCCR-Mageuzi Julai 18, 1994 akiwa mwanachama kutoka Jimbo la Kasulu Vijijini Mkoani Kigoma. Alikabidhiwa kadi ya Uanachama yenye namba 006759.

Katika kipindi cha Mwaka huo wa 1994, Mzee Maganga alishika nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa mipango na Uchaguzi Wilayani kasulu, Mkoani kigoma mpaka 2014.

Akiwa ndani ya chama cha NCCR-Mageuzi amefanikiwa kupata Semina tofauti za kiuongozi, kutembea Mikoa tofauti kujifunza jinsi wanachama wa NCCR Mageuzi wanavyoishi pamoja na kutembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuweza kufahamu namna ya wawakilishi wao wanavyofanya kazi.

Safari yake kisiasa haikuwa nyepesi kwakuwa aliwahi kupelekwa Mahakamani zaidi ya mara 10 kwa kutetea chama chake pamoja na kukamatwa na Jeshi la polisi mara kwa mara katika harakati za kukijenga chama.

Mnamo mwaka 2015 alijiunga na chama cha ACT-Wazalendo baada ya kuombwa na familia yake kwenda kuweka nguvu kwa kijana wake Emmanuel Thomas Msasa aliyekuwa mgombea Ubunge jimbo la kasulu Vijijini.

Mzee Maganga alikubali kufanya hivyo kwa shingo upande huku nafsi yake ikimsuta kwakuwa alikuwa akizikumbuka fadhila zilizokuwa zinafanywa na ndugu James Mbatia (Mb) kwa wanachama wa NCCR-Mageuzi.

Mzee Wiliam Maganga kushoto akiwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi wa Taifa na Mbunge wa Jimbo la Vunjo ndugu James Mbatia (Mb) kulia.

Narudi kwenye nyumba niliyoianzisha

Akiwa kama mwanachama wa ACT-Wazalendo, Mzee William Maganga amekiri kuwa ameona mambo mengi ambayo hakupendezwa nayo ikiwa ni pamoja na ubinafsi kwani aliwahi kugombea Ngome ya wazee ngazi ya Taifa ambapo fomu yake ilitupwa kapuni.

Mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, Ndugu Willium Maganga Kasabage aliamua kutamka rasmi kuwa “Ninarudi kwenye kwenye nyumba aliyoiasisi ya NCCR Mageuzi” kauli hii inathibitisha wazi kuwa sasa Mzee Maganga ameamua kuachana na ACT-Wazalendo na kurejea nyumbani NCCR-Mageuzi.

“Nimeona ni bora nirudi kwangu kwenye nyumba niliyoianzisha, ni bora nikazibe nyufa nirudi mahala pake, viongozi wa NCCR naomba mnipokee naomba niwe mtu wenu kwa maisha yangu yote”-Alisema mzee Maganga

‘Ninarudi NCCR Mageuzi kutokana na chama hiki kuishi itikadi ya UTU na ndicho chama pekee kinachojituma kwa maslahi ya Watanzania wote”-Alisema

Mzee William Maganga anaamini chama cha NCCR Mageuzi kinarudi kuwa kwenye ushindi mkubwa.

Chama chetu cha NCCR-Mageuzi kinaamini kuwa njia bora ya kuleta mageuzi na kuongoza serikali kutaleta mabadiliko katika jamii yetu kwa kuwa na amani, hiari na nguvu ya hoja itokanayo na itikadi ya sera zetu zinazolenga kuwakomboa wanyonge wapate maendeleo na ustawi.