•  Akwepa kushambulia Chama chake cha zamani.

  • Aahidi kuhimiza watendaji kutekeleza agizo la Rais Magufuli.

 

Na mwandishi wetu, Kigoma.

Aliyekuwa mwanasheria mkuu wa chama cha ACT wazalendo, ndugu Thomas Msasa amejiunga rasmi na chama cha NCCR-Mageuzi na kuahidi kushirikiana nao kuhakikisha kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu mwaka huu 2020.

Akizungumza wakati wa kupokea kadi ya chama hicho mjini Kasulu mkoani Kigoma leo Ijumaa 05/06/2020 amesema amejiunga NCCR-Mageuzi baada ya kutafakari kwa kipindi cha mwezi mmoja ajiunge na chama gani.

“Nilitangaza kujivua uanachama wa ACT-Wazalendo 05/05/2020 na katika kipindi hicho chote nilikuwa natafakari ni chama gani ambacho naweza kujiunga kwa ajili ya kuendeleza harakati za kisiasa, na hatimaye nilibaini NCCR ndio inayonifaa,” amesema Msasa.

Tofauti na wanasiasa wengi wanaohama vyama vyao hususani viongozi, wabunge na madiwani ambao wana tabia ya kutoa lugha za matusi na kashfa kwa vyama vyao vya zamani, Msasa hakutaka kuzungumza chochote kibaya dhidi ya ACT wazalendo.

“Sitaki kuongea jambo lolote baya na uozo uliopo katika baadhi ya vyama vya siasa kwa sababu itakuwa ni sawa na kujivua nguo, muhimu tushirikiane kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi,” amesema Msasa.

Aidha ameomba watendaji wa serikali kutekeleza agizo la Rais John Magufuli alilotoa mwaka 2017 kuhusu mgogoro wa wakulima wanaolima ndani ya hifadhi ya msitu wa Makere kusini katika eneo la Kagerakanda, ambapo alitaka wapewe eneo wanalolima.

Rais akiwa katika ziara ya kikazi aliagiza watendaji wa serikali ngazi ya mkoa wa Kigoma na wilaya ya Kasulu kupima upya maeneo ya hifadhi hiyo na kuwaachia wakulima waendelee kulima katika eneo walipovamia na kulima.

“Kagerakanda wakulima wanateseka sana, wakati wa kulima hakuna anayeulizwa lakini inapofikia kipindi cha mavuno ndio askari wanazuia mabarabarani na kuwanyang’anya mazao yao, huu ni ukatili na hauwezi kuvumiliwa. Lazima agizo la Rais litekelezwe,” amesema Msasa.

Aidha amewataka viongozi wa serikali kuhakikisha watu waliojenga pembeni ya barabara ya Kabingo hadi Kibondo inayofadhiliwa na Benki ya Afrika (AfDB) wanalipwa fidia ya mali zao kabla ya mradi haujaanza kujengwa kama mkataba unavyoelekeza.

Kamishna wa NCCR mageuzi mkoa wa Kigoma, ndugu Danford Kagabo amesema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha wanashinda kwenye uchaguzi mkuu kwa kupata wabunge na madiwani wengi kadri inavyowezekana.

“NCCR imejiandaa kushinda katika majimbo yote manane mkoani Kigoma huku akiwaomba viongozi kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano kwa faida ya wapenzi wa vyama vya siasa,” amesema Kagabo.

Mwenyekiti wa NCCR jimbo la Kasulu vijijini, Ignas Mahoga amesema chama hicho kitaendelea na itikadi yake ya utu na kujali haki ya kila mmoja.