Kufuatia uharibifu mkubwa wa miundo mbinu pamoja na makaazi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kata ya Kahe, Jimbo la Vunjo, Wilaya ya Moshi, Mbunge wa Jimbo la Vunjo ndugu James Francis Mbatia amemtuma katibu wake kutembelea eneo hilo na kufanya tathimini ya athari zilizojitokeza.

Akiongea na mwandishi wetu, Katibu wa Mbunge wa Jimbo hilo ndugu Daniel Shayo amesema, kuendelea kwa vikao vya Bunge pamoja na kutokea kwa vifo vya baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mbunge huyo ameshindwa kufika katika eneo hilo na hivyo kumtuma kuja kufanya tathimini ya athari iliyojitokeza.

Diwani wa kata ya Kahe, Ndugu Lodrick Mmanyi akiwa na timu ya Mbunge wa Jimbo la Vunjo ndugu James Mbatia katika kuangalia na kutathimini athari za mafuko kwa wakaazi wa kata hiyo.

Pamoja na kufanya tathimini ya uharibifu katika eneo hilo, lakini pia Mbunge wa jimbo hilo ndugu James Mbatia ametoa msaada wa mavazi kwa kaya ambazo zimepoteza baadhi ya vitu vyao ikiwa ni msaada wa awali wa kulinda UTU wa binadamu ili kuweza kujisitiri wakati tathimini ikiendelea.

Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zimeleta athari kubwa kwenye eneo la mto wa Nafco ambao unatumiwa na Wakulima wa kikundi cha Mawala (Mawala Scheme) pamoja na TPC ikiwa ni pamoja na kuharibu barabara inayounganisha kijiji cha Kisangesangeni kwenda kata ya Kirua-Vunjo Kusini.