Siku takribani 90 zimesalia kabla ya watanzania kufanya maamuzi kwenye sanduku la kupiga kura hapo Oktoba 28, 2020. Kinachozungumzwa sasa sio hiyo siku yenyewe ya uchaguzi, la asha bali ni nani atakuwa nani? Nani atakuwa jimbo gani na nani atakuwa kwenye kata gani?

Chama cha NCCR-Mageuzi kuelekea uchaguzi wa mwaka huu kimejipanga kufanya makubwa na yatakayofunga midomo ya walio wengi. Idadi ya wanachama pamoja na watia pia inaakisi lengo na dhumuni la kuchukua dola.

Julai 29, 2020, Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi Taifa ndugu James Francis Mbatia amepokea wanachama wengine wapya ambao wanatajwa kuwa na nguvu kwenye majimbo wanayowakilisha. Moja ya mtia na mwanachama mpya aliyepokelewa ni Bi. Aurelia Steven Kibona.

Bi. Aurelia Steven Kibona ni mtoto wa waziri wa fedha wa zamani, marehemu Steven Kibona aliyehudumu kwenye nafasi ya uwaziri wa fedha katika kipindi cha utawala wa Rais Mstaafu Ally Hassan Mwinyi.

Mbali na kuchukua kadi ya uanachama ndani ya NCCR-Mageuzi, Bi. Aurelia Kibona amechukua fomu ya kutia nia kugombea Ubunge kwenye Jimbo la Ileje, mkoa wa Songwe nyanda za juu kusini.

Ndugu Martin Mng’ong’o ambaye ni mkuu wa Idara ya Kampeni na uchaguzi ndani ya NCCR-Mageuzi amemkabidhi rasmi fomu ya Ubunge Bi. Aurelia Kibona pamoja na wananchama wapya wengine wawili akiwemo Bi. Olivia Chagula ambaye amechukua fomu ya ubunge wa viti maalum Jimbo la Kawe.

Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi ndugu Martin Mng’ong’o akimkabidhi fomu ya Ubunge Bi. Aurelia Steven Kibona.

NCCR-Mageuzi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba imejipanga kikamilifu kuhakikisha inashika dola pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wawakilishi bungeni na kwenye baraza la madiwani.