• Abdul Nondo bado mchanga kisiasa
  • Achunge kauli zake
  • Aepuke kutumiwa na viongozi wa chama chake

Na mwandishi wetu, Kigoma.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Jimbo la Kigoma mjini, Wiston Andrew Mogha amesema Chama cha ACT Wazalendo kilitumika kuisaidia CCM kushinda katika uchaguzi mkuu mwaka 2015, na hivyo kupunguza nguvu ya vyama vilivyounda UKAWA.

Mogha ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Mei 26, 2020 katika ofisi ya chama cha NCCR-Mageuzi Mjini Kigoma alipokuwa anazungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Alitumia nafasi hiyo pia  kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa wa chama cha ACT wazalendo, Abdul Nondo aliyezungumza na waandishi wa habari jana Jumanne mjini Dar es salaam.

Amesema CCM waliomba chama cha ACT kiweke mgombea urais ili kisaidie kupunguza kura za mgombea wa Chadema na muungano wa UKAWA, Edward Lowasa.

Pia Lowasa aliwaomba viongozi wa ACT wasiweke mgombea urais bali wasimamishe wagombea ubunge na yeye (Lowasa) angewashawishi viongozi wa vyama vilivyounda UKAWA kuwaachia ACT majimbo kumi na kusaidia kuwapigia kampeni wagombea hao.

“Baada ya maombi hayo mawili ACT walikubali kuisaidia CCM na ndipo walipoamua kumteua aliyekuwa Mwenyekiti wake, Anna Mghwira kuwa mgombea urais. Lengo likiwa ni kupunguza kura za Lowasa na UKAWA kwa jumla,” amesema Mogha.

“Sasa katika mazingira haya ni chama gani kati ya NCCR mageuzi na ACT wazalendo kinatumiwa na CCM?” amehoji Mogha.

Aidha amemtaka mwenyekiti wa ngome ya vijana Taifa wa chama cha ACT wazalendo, Abdul Nondo kuacha tabia ya kutoa maneno ya dharau na kashfa kwa chama hicho, badala yake kila mmoja ajenge chama chake.

“Nondo bado ni mchanga kisiasa ndio maana anaongea maneno asiyojua, na anapoishutumu NCCR kuwa inatumiwa na CCM ni kuwakosea adabu viongozi na wanachama wa chama hicho,” amesema Mogha.

Kuhusu madai ya Nondo kwamba NCCR Kigoma mjini kuna vijana wawili tu na chama hakina hata kamati ya utendaji, vijana hao kutamba kwenye mitandao ya kijamii kwamba chama kinakua huku akisema chama hicho ni kundi la watu wenye maslahi binafsi, Mogha amekanusha madai hayo.

“NCCR inatumia haki yake kikatiba kujijenga kisiasa, lakini kuna watu wanaanza kutuchokoza. Sisi tunajua mengi ya ACT na hatupendi kusema lakini leo tumeongea kidogo tu ili waache kutuchokoza, hatuna ugomvi nao wowote ule kisiasa,” alisema.

Amesema kwa sasa NCCR inajijenga upya baada ya kubaini makosa yaliyofanywa kutoka kuwa chama chenye nguvu kisiasa nchini na kubaki cha kawaida miaka michache baadae. Kigoma viongozi wamekamilika.

Amesema uchaguzi wa mwaka 1995 kilipata wabunge 16 na mwaka 2000 kikapata mbunge mmoja, Kifu Gulamhussein. Mwaka 2005 kulikosa kabisa mbunge.

Mwaka 2010 kikapata wabunge wanne kutoka majimbo ya mkoa wa Kigoma ambao ni David Kafulila, Moses Machali, Zaituni Buyogela na Felix Mkosamali.

“Baada ya kupata mbunge mmoja mwaka 2015 imebidi kujipanga upya na kuweka mikakati mizito ya kupata wabunge wengi mwaka huu 2020 na watu wanavutiwa na mikakati yetu, ndio maana wanakuja kujiunga,” amesema Mogha.

Ametoa mwito kwa viongozi vijana kuacha tabia ya kubeba agenda za viongozi wao wakubwa katika vyama vyao kwa vile matokeo yake ndio hayo ya kutoa lugha chafu na kudhalilisha wengine bila hatia.

NCCR-Mageuzi haitishwi na maneno ya viongozi au wafuasi wa vyama vingine bali wamejikita kuhakikisha wanajenga imani kwa wapiga kura ili waweze kushinda katika uchaguzi mkuu kwa kupata wabunge na madiwani wengi, ikibidi hata kushinda urais wa nchi.