Siku moja imepita sasa tangu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Ndg.  James Mbatia alipokuwa akihojiwa na chombo cha habari cha Mwananchi Communication, kwenye mahojiano ambayo yalikuwa Mubashara kupitia Mtandao (Online Television). Agenda zikiwa ni maswali mengi yanayoibuliwa sasa hasa kuelekea kwenye kipindi cha uchaguzi utakaofanyika mapema mwaka huu. Baadhi ya mambo/hoja zilizojadiliwa na kutolewa ufafanuzi na Ndg. James Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo ni pamoja na,

 1. James Mbatia kudhuru Ikulu kwa mazungumzo na Mh. Rais.

Moja ya hoja zilizoibuliwa kwenye mahojiano hayo ni pamoja na mualiko wa Ndg. James Mbatia na baadhi ya viongozi wa vyama vingine vya siasa nchini kwenda Ikulu mnamo Machi, 3, 2020 kuzungumza na Mh. Rais John Pombe Magufuli.

Majibu ya hoja hii ambayo yalijibiwa moja kwa moja na Ndg. James Mbatia yalikuwa kama ifuatavyo;

“Kupitia jukwaa la vyama vya siasa vilivyo na uwakilishi Bungeni tulikuwa na maazimio kadhaa, na moja la azimio ni kumuomba Mhshimiwa Rais tuweze kufanya mazungumzo na mjadala wa maridhiano”

“Mkutano tulioufanya juzi Ikulu ulitokana na juhudi za kuendelea kumkumbusha Mh. Rais zaidi ya mara mbili tuweze kufanya mazungumzo ya maridhiano kokana na hali iliyopo sasa ya kisiasa”

Mazungumzo na Makubaliano kati ya Mh. Rais pamoja na Ndg. James Mbatia

 • Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa kauli aliyoitoa kwa mabalozi mbalimbali juu ya kuwepo kwa Uchaguzi wa huru na haki ilikuwa ni thabiti na Serikali italisimamia hilo kwa dhati
 • Masuala ya huduma za kijamii kwenye jimbo la Vunjo ambapo Ndg. James Mbatia ndio Mbunge
 • Jambo lolote linalofanywa basi lizingatie Maslahi ya Tanzania
 1. Suala la uwepo wa Tume huru ya Uchaguzi

Suala la uwepo wa Tume huru limekuwa na mjadala endelevu kila kukicha, lakini kupitia mjadala dhidi ya waandishi wa habari, Ndg. M/kiti James Mbatia alisisita kuwa,

Tangu kuasisiwa kwa NCCR-Mageuzi tarehe 12, Juni, 1991, msimamo wa chama ni kuwa na katiba mpya yenye kufuata mfumo wa demokrasia ya vyama vya siasa. Tume ya uchaguzi ni sehemu ya katiba. Msimamo wa chama ni kuwa na katiba mpya pamoja na makubaliano ya namna gani ya kufanya uchaguzi, pamoja na kuwa na Tume ya uchaguzi inayokubalika na pande zote.

 1. Ushirikiano wa vyama vya Siasa

Suala la ushirikiano wa vyama vya siasa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Ndg. James Mbatia amesema kuwa, wanaunga mkono mashirikiano ya vyama vya siasa na wala hawajawahi kutoa tamko la kuwa wao wanakataa au wanatoka kwenye ushirikiano wa vyama.

 1. Suala la kubadilisha sheria ya Uchaguzi

Mwenyekiti amesema moja ya maazimio ambayo waliyatoa Bungeni hapo siku za nyuma ni pamoja na kufanya mabadiliko ya sheria za Uchaguzi (Minimum Reforms) endapo tu Katiba mpya itashindikana. Baadhi ya maazio/mabadiliko hayo ni pamoja;

 • Ili Rais aweze kuchaguliwa lazima apate zaidi ya 50% ya kura
 • Kuwe na tume ya ridhaa ya wananchi na inayoonyesha utaratibu muafaka
 • Matokeo ya Rais yaweze kuhojiwa Mahakamani
 • Suala la Mgombea huru

Hizo ni baadhi tu ya hoja zilizojadiliwa kwenye mahojiano hayo ambayo yalikuwa mubashara kupitia Mwananchi Media.