Oktoba Mwaka huu ni siku ambayo Watanzania watachagua viongozi watakaoliongoza Taifa hili kwa kipindi kingine cha miaka mitano, kwa kuwapigia kura katika ngazi ya Urais, Ubunge pamoja na Udiwani.

Huu ndio muda muafaka kwa Wanawake wa chama cha NCCR-Mageuzi kujitokeza kugombea katika nafasi mbalimbali ndani ya chama ili kuweza kutoa mchango wao chanya kwa maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na kusemea changamoto za akinamama na Watoto wa taifa hili kwa kusimamia misingi ya Itikadi ya UTU.

Ni ukweli usiopingika kofia ya Wanawake wa Mageuzi ikivaliwa vizuri itaongoza taifa kwa weledi mkubwa  kwa kusimamia na kutetea haki msingi kwa makundi yote ndani ya Taifa hili kwa kuzingatia usawa wa jinsia na misingi ya itikadi ya UTU kwa maslahi ya mama Tanzania.

Ni wazi Uwakilishi wa wanawake katika ngazi za maamuzi katika serikali iliyopita kumechangia kwa kiasi kikubwa wanawake wengi kujitokeza katika uchaguzi wa mwaka huu kuwania nafasi tofauti za uwakilishi ili kutatua changamoto katika jamii.

Hivi karibuni Wanawake ulimwenguni wameendelea kwa namna tofauti kupigania usawa wa kijinsia ili kuifikia asilimia 50/50 katika ngazi zote za maamuzi kwa kuwa na dunia yenye misingi ya Usawa na uwajibikaji.

Hata hivyo kulingana na Umoja wa Mataifa{UN Women}unabainisha vikwazo viwili vikuu vya kimuundo ambapo sheria baguzi na taasisi bado zinabana uwezo wa wanawake kugombea nafasi za kiungozi.

Ikumbukwe kuwa Wanawake wa Mageuzi hawana budi kuwa wamoja kwa kuyaenzi mazuri yaliyofanywa na wanawake wa taifa hili kwa kutoa hoja kwa kielelezo huku sera ya Umoja ni nguvu Utengano ni Udhaifu kutachagiza kutwaa Ushindi na kuwapata viongozi wanawake wenye mapenzi mema na taifa.