Joseph Roman Selasini ni mbunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwakilisha wananchi wa jimbo la Rombo mkoa wa Kilimanjaro kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

April 28,2020 Joseph Selasini ameweka bayana kuwa atarajea kwenye chama alichokiasisi cha NCCR-Mageuzi chama ambacho alikipigania katika harakati za kudai Mabadiliko na kurejea Juni 30 mwaka huu.

Katika harakati zake Selasini alijiunga na vuguvugu la kupigania chama cha NCCR-Mageuzi kwenye mfumo wa vyama vingi nchini, mwanzoni wa miaka ya 1990, wakati huo akiwa mwajiriwa wa Benki ya Nyumba Tanzania (THB) katika nafasi ya Meneja wa Utawala na uendeshaji. Alitenga muda wake wa likizo, siku za mapumziko na rasimali zake binafsi kuchangia harakati za kutetea Demokrasia, uhuru wa kujieleza na kustawi kwa mfumo wa vyama vingi kunafanikiwa.

Mnamo mwaka 1992 akiwa bado mfanyakazi wa THB, aliteuliwa na chama kuwa Katibu wa Vijana wa NCCR- Mageuzi, chini ya Uenyekiti wa ndugu James Francis Mbatia.   Ushiriki wake kwenye harakati za mageuzi ulisababisha kufukuzwa kazi mwaka 1993 kwa mizengwe iliyokuwa nyuma ya pazia la siasa za upinzani.

Baada ya kufukuzwa THB aliamua kufanya siasa moja kwa moja na kuteuliwa kuwa Afisa Tawala wa Chama   Makao Makuu ya NCCR- Mageuzi, huku Mkurugenzi wangu akiwa  ndugu Anthony Calist Komu na baadaye niliteuliwa kuwa Katibu Mwenezi wa Taifa.

Mbunge wa Jimbo la Rombo Ndugu Joseph Selasini akizungumza na waandishi wa habari

Mnamo mwaka 2010 na 2015 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Rombo kwa vipindi viwili mfululizo kwa tiketi ya CHADEMA.  Wakati anagombea Ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2010 Jimbo la Rombo lilikuwa na diwani mmoja wa kutoka CHADEMA kwa sasa kuna madiwani wa kuchaguliwa 27 kati ya 28 na 10 wa viti maalum na kuongoza Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mafanikio haya makubwa yaliyopatika kwa kushirikiana na wapenda mageuzi.

Mnamo mwishoni mwa mwaka 2017 alichaguliwa kuwa  Kaimu Mwenyekiti wa Mkoa wa Kilimanjaro na Kanda ya Kaskazini  mpaka Desemba 2019. Pia aliteuliwa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni kuwa Kaimu Mnadhimu wa Upinzani Bungeni tangu mwishoni mwa mwaka 2017 mpaka Januari 2020 alipoamua kujiuzulu nafasi hiyo.

Pamoja na yote haya, ndugu Selasini amekutana na changamoto nyingi kutoka ngazi ya Taifa kwa kuwa aliona ni wajibu wake kufanya kazi bila kinyongo. Siku zote alipuuza maneno na mizengwe dhidi yake kwa kuwa zilikuwa changomoto za kisiasa, pamoja na hayo yote tarehe 25.04.2020 siku ya jumamosi alitolewa katika group la (WhatsApp) ambalo ni nyenzo muhimu ya kazi na uongozi shirikishi ndani ya chama chake bila taarifa; hii ni sawa na kusema akufukuzae hakwambii toka;

Mwenyewe anasema alipoasisi Mageuzi, alikuwa anapigania haki ya kuchagua na kuchaguliwa na kukiri kuwa haki hiyo, haipo ndani ya Chadema ya sasa. Na kusema kuwa kwa sasa, ndani ya Chadema, kuna kikundi cha watu ndicho kinachoamua nani awe kiongozi na nani asiwe kiongozi hili linaudhi sana na mifano ipo mingi.

Ananukuliwa “wakati tunaanzisha mageuzi tulihubiri kwa sauti kubwa, kwamba “Tunataka Vyama Vingi, na kwamba upinzani siyo uadui.” Tuliamini: “Tutapingana bila kupigana.” Alisema Ndugu Joseph Selasini.

Hivi sasa Malengo haya hayapo ndani ya Chadema, na kwamba ndani ya Chadema, mpinzani wa kweli, ni yule anayekuwa tayari kupotosha ukweli kwa sababu tu nilazima kupinga kila kitu-Alisema

“Serikali ikijenga hospitali jimboni kwako au reli, basi wewe uwe tayari kusimama hadharani na kusema, “serikali haijafanya kitu, hawajui kunatofauti ya Serikali na chama cha siasa.” Alisema Ndugu Joseph Selasini

Amesema ukitaka kupendwa na viongozi wakuu wa Chama, sharti uwe tayari kuimba kile mwandishi wa habari za kwenye mtandao, ndugu Ole Mushi anakiita, “ litania ya Mwamba Tuvushe, na kwamba bila yeye hakuna Chadema, kwa msingi huu hiki sio chama cha siasa. Nje ya wimbo huo, unachukiwa, kusimangwa na kutengwa. Hivyo ndivyo nilivyoishi mimi ndani ya Chadema kwa miaka 12 ya uwanachama wangu. Nguvu ya kunivuta nirudi kwenye asili ya Mageuzi ni kubwa mno, ukichanganya na msukumo wa kuikimbia CHADEMA;

Nguvu hiyo ya mageuzi imempelekea kuutangazia umma kwa hiari yake mwenyewe kwamba hawezi kukubali kuendelea kujifunga katika kitu ambacho hakiamini. Na kusema kwamba mara baada ya kumaliza kipindi chake cha ubunge, atarejea kwenye chama alichokiasisi cha NCCR- Mageuzi, ambacho ndiyo baba na mratibu wa ujio wa mfumo wa vyama vingi hapa nchini Tanzania.

Mbunge wa Jimbo la Rombo Ndugu Joseph Selasini akizungumza na waandishi wa habari

Ndugu Joseph Selasini anatambua katika dunia ya leo, ukuu wetu katika kutumikiana umejikita katika mambo yafuatayo, ambayo yanapatika ndani ya NCCR – Mageuzi pekee.

  1. Kujali uumbaji wa Mwenyezi Mungu – Hii imejikita kwenye itikadi ya UTU, tofauti na itikadi za vyama vingine.
  2. Utambuzi wa usawa wa Binadamu . Ukianza na usawa wa jinsia na hii iko kwenye nembo ya NCCR – Mageuzi na inatekelezwa kwa vitendo, kuna picha ya Mwanamke na Mwanaume kuonesha uhalisia.
  3. Kushirikiana ndiyo ushindi. Kauli mbiu ya NCCR – Mageuzi ni “Pamoja Tutashinda” NCCR – Mageuzi inatoa uhuru wa kushirikiana na Mtanzania yeyote wenye kujali maslahi mapana ya nchi yetu , Ndani ya CHADEMA ukijaribu hili unaitwa msaliti.
  4. Maisha yamo vinywani mwetu. Lugha ya NCCR – Mageuzi ni ya kujenga kwa kuzingatia Utu wanaitana ndugu na siyo waheshimiwa. Hata wanapoumizwa wanamtangulinza Mwenyezi Mungu alinde ndimi zao kwa maslahi ya Mama Tanzania.
  5. Katiba ya Chama ni makubaliano ya wote hivyo lazima ifuatwe kama inavyofanya NCCR-Mageuzi hasa katika Itikadi yake ya UTU, Malengo ya Kisiasa, Madhumuni ya Chama, Sifa za Kiongozi, Haki za mwanachama hizi nimetaja kwa uchache.

Itakumbukwa kuwa ndugu Selasini ni kiongozi anayejitoa, mvumilivu, anajituma, na yupo mstari wa mbele kutoa msaada unapohitajika.