Kufuatia kuwepo kwa visa kadhaa vya wagonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19) nchini, jamii imeshauriwa kuwa makini hasa katika kusikiliza yale yanayoelekezwa na wataalamu kuhusiana na ugonjwa huo.

Tayari visa kadhaa vya wagonjwa wa homa ya mapafu vimetajwa nchini huku tahadhali zikiendelea kuchukuliwa na kila mmoja katika kuhakikisha maambukizi ya virusi vya Corona yanapungua au kumalizika kabisa. Akitoa rai kwa watanzania wote Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi na Mbunge wa jimbo la Vunjo Mkoani Kilimanjaro ambaye pia ni mtaalamu wa majanga Ndg. James Francis Mbatia  amesema,

“Linapotokea janga, inabidi kuwa na sauti moja na timu moja na kutekeleza yale tunayoelekezwa”

Kwa upande mwingine Ndg. James Mbatia ameiomba serikali kutumia vyombo vya habari nchini katika kutoa elimu kwa jamii namna iliyo bora ya kujikinga na virusi hivi vya Corona ambayo vimekuwa tishio sasa ulimwenguni. Lakini pia ameziomba taasisi za dini kutumia nafasi yao katika kuihasa jamii kuchukua tahadhali dhidi ya virusi vya Corona ikiwa ni pamoja na kufuata maelekezo sahihi kutoka kwa wataalamu.

Mlipuko wa maambukizi ya corona umeathiri mataifa mbalimbali duniani. Mpaka saa nchini Tanzania visa kadhaa vimetajwa vya wagonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19). Hali ya tahadhali inazidi kuchukuliwa huku Wataalamu wakisisitiza kuwa na usafi wa mara kwa mara kwa watu kuosha mikono yao kwa maji na sabuni, kutumia vitakasa mikono na kutojigusa mdomoni.