Nchi yetu inajiandaa kufanya Uchaguzi mkuu wa Udiwani/Wawakilishi, Ubunge pamoja na Urais ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu. Vyama vingi vya siasa vimeendelea kupoteza wanachama na hasa wanachama wanaotajwa kuwa ni nguzo katika siasa za vyama vyao kuanzia ngazi ya kijiji, kata, jimbo na hata Taifa. NCCR-Mageuzi kwenye uchaguzi huu ndio chama pekee kinachowapokea wanachama wengi kutoka vyama vingine vya Siasa nchini hasa vile vya Upinzani, hali inayoibua malalamiko yasiyokuwa na tija kwenye nchi inayojali demokrasia yanayolenga kukichafua chama. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa fursa na Uhuru kwa mtu yeyote au mwanachma yeyote kujiunga na chama chochote cha Siasa.

Akiongea mbele ya waandishi wa habari mjini Dodoma Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa ndugu James Francis Mbatia, amesema anashangazwa na watu wanaolalamika juu ya chama hicho kupokea wimbi la wanachama wanaojiunga na NCCR-Mageuzi ambayo Itikadi yake ni ile yenye kujali UTU. Ndugu mwenyekiti amesema hili si jambo la kushangaza au kuanza kurusha maneno ya hovyo ikiwa mwasisi namba moja wa chama cha NCCR-Mageuzi ambaye ana kadi ya Uanachama namba moja alikihama chama hicho na kujiunga na chama kingine cha Upinzani (CHADEMA).

“Mimi ni Mbunge wa Vunjo, uliwahi kusikia hata siku moja nalalamikia kwanini CHADEMA waliweka mgombea kule Vunjo? niwe mkweli Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, vyama vingine waliweka wagombea tukiwa kwenye UKAWA kule Vunjo tukagawana kura za Madiwani, madiwani wengine wa CCM wakashinda, ulisikia nimelalamika popote?”-Alisema Ndugu James Mbatia.

Kwa upande mwingine ndugu James Mbatia alitoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na Ushirikiano wa vyama ambao hakusita kusema kuwa chama cha NCCR-Mageuzi suala la ushirikiano ni kipengele kilichopo ndani ya katiba ambapo inakitaka chama si tu kushirikiana na chama pekee lakini pia kushirikiana na watu na hata jamii.

“NCCR-Mageuzi sio kwamba tu tunataka kushirikiana na vyama, iko ndani ya katiba, na katiba yetu inasema wazi kabisa, tutashirikiana na jamii, tutashirikiana na watu na tutashirikiana na vyama vingine vyenye madhumuni na malengo yanyofanana na sisi.”

Chama NCCR-Mageuzi kwa kimejikita katika ujenzi wa Chama kupitia Itikadi ya UTU ambayo inaonyesha kukubalika sana nchini kutokana na misingi yake inayozingatia, uawa haki, udugu maadili, uhuru, mabadiliko n.k