Ni zaidi ya miaka 20 sasa tangu Tanzania ingiie katika mfumo wa Demokrasia ya vyama vingi. Ni dhahiri nchi yetu iko katika kipindi cha demokrasia ya mpito (democratic transition) kuelekea demokrasia kamili (democratic consolidation). Tayari zimepita chaguzi 5 tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi, lakini pamoja na ukweli kuwa chaguzi zote kuu 5 zimeendeshwa katika mazingira ya amani na utulivu, bado kumekuwa na malalamiko, hasa kwa vyama vya upinzani juu ya mazingira ya ukuaji wa demokrasia kwa ujumla.

Kupitia mjadala ulioendeshwa na Kituo cha Demokrasia nchini (TCD) chini ya mwenyekiti wake Ndg.  James Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Mbunge wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, wakishirikiana na The Open Society initiative For Eastern Africa (OSEA), wajumbe na washiriki wa mjadala kutoka kwenye vyama mbalimbali vya siasa pamoja na taasisi wameazimia kuwepo na mjadala wa maridhiano baina ya vyama vya siasa. majadiliano hayo yanapaswa kuzingatia hoja takribani 16 ambazo ni

Majadiliano ya vyama vya siasa yazingatie mambo haya;

 1. Uundwaji wa katiba mpya
 2. Tume huru ya Uchaguzi
 3. Ruzuku kwa vyama vya siasa
 4. Uhuru wa vyama vya siasa kufanya kazi zake za kisiasa
 5. Uboreshaji wa demokrasia ya vyama vingi
 6. Ushirikiano baina ya vyama vya siasa katika kuimarisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
 7. Utoaji wa elimu ya siasa kwa raia
 8. Umuhimu wa waandishi wa habari katika shughuli za siasa
 9. Uandaaji wa chaguzi huru na za haki
 10. Wagombea huru
 11. Muungano wa vyama katika kusimamisha mgombea mmoja katika ngazi ya Uais
 12. Kuachiana majimbo katika uchaguzi wa wabunge na madiwani
 13. Waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje
 14. Haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi Mahakamani
 15. Utatuzi wa migogoro
 16. Changamoto za ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma bora za jamii kwa wananchi.

Katiba inayotumika sasa ni ile ya mwaka 1977 ambayo imefanyiwa mabadiliko zaidi ya mara 10, lakini bado malalamiko yapo mengi. Hata hvyo baadhi ya viongozi waliwahi kutoa mapendekezo yao ya namna ya kupitisha ajenda au sheria za uchaguzi kuelekea uchaguzi mkuu 2015 endapo nchi itashindwa kupata katiba mpya kabla ya uchaguzi. Hoja 16 zilizowekwa mezani kwa sasa na wajumbe ni tosha kuna mabadiliko makubwa yanahitajika kwenye sheria ya uchaguzi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.