Mjadala: ‘Haki ya elimu bure’ (right to free education) kwa kunzingatia mfumo wa kisheria na kimantinki katika upatikanaji wa elimu bora, jumuishi na sawa kwa wote.
Swali: ‘ni hatua gani tumefikia katika kufanikisha haki ya elimu bora, jumuishi na sawa kwa wote?
Ninaomba sisi tuliojumuika hapa tutafakari kidogo juu ya hali ya elimu yetu hapa Tanzania, dhima yake na matokeo ya elimu hiyo kwa taifa.
Swali: wangapi kwa wastani wanaridhishwa na hatua tuliyofikia katika upatikanaji wa elimu bora, jumuishi na sawa kwa wote?
Pamoja na kwamba mjadala utagusia mambo kama ada ya elimu, uandikishaji na ufaulu wa wanafunzi, ubora wa walimu na miundombinu ya kujifunzia; mimi nitajikita zaidi kwenye kuzingatia upatikanaji wa elimu bora.
Swali: Je, elimu ya namna hii inatusaidia vipi katika kujitambua hasa tukizingatia historia ya kutawaliwa kisiasa na kiuchumi?

 • kujitambua kwa maana ya kujua uwezo wetu kama taifa na uwezo wa kila mmoja wetu wa kujikomboa kifikra, SOTE TUNAWEZA;
 • kujitambua kwa maana kuheshimu haki msingi za binadamu zitokanazo na maumbile na mazingira yake (mazingira yanayobadilika kwa kasi ya kuendana na ukuaji wa teknolojia duniani);
 • kujitambua kwa maana ya kuweza kutumia rasilimali tulizonazo ili tuishi maisha yenye furaha;
 • kujitambua kwa maana ya kuweza kubeba wajibu wetu, kama taifa, wa kushiriki katika maswala mbalimbali ya kimataifa;
 • kujitambua kwa maana ya kukubali uwezo wa mwanadamu kukua (human evolution).
  Swali: Katika safari hii ya kukuza uwezo wa mtanzania wa kujitambua na kujikomboa kifikra, tunathubutuje, kuwakusanya baadhi ya watoto wetu kwenye mazingira ya kudhalilisha ubinadamu wao? mazingira ya kuwanyima haki msingi ya kibinadamu? haki ya kutumia Choo!
  Wale wenye dhamana serikalini huwajibika kuonesha hatua zilizofanyika katika utoaji wa elimu, kwa mfano:
 • uzuri wa sera;
 • ubora wa mtaala, mihutasari ya masomo na vitabu;
 • ongezeko la kiasilimia la uandikishaji na ufaulu wa watoto shuleni;
 • ongezeko la walimu,
 • ongezeko la bajeti ya elimu,
 • ongezeko la miundombinu ya madarasa na nyumba za walimu
  nikitaja kwa uchache ili kuonesha kwamba tunaendelea vizuri na utoaji wa elimu;
  Swali: Je, hatua hizi zimetupa uwezo wa kujitambua na kujikomboa kifikra?
  Kwa kweli changamoto zipo. Baadhi ni za kujitakia na baadhi zinatokana na mabadiliko ya kiulimwengu.

Kwa mfano,

 • udhaifu katika sekta ya elimu hapa Tanzania, hasa katika ubora wa sera, mtaala, mihutasari na vitabu vya kiada na ziada unatokana na maamuzi ya kisiasa zaidi bila kuzingatia taaluma husika. Mfumo shirikishi na endelevu haupo.
 • mabadiliko ya tabia nchi, mfumo wa uchumi duniani na ukuaji wa teknolojia yanaleta changamoto za kimataifa ambazo bado tunawajibika kuzishughulikia. Hii ni sehemu ya kuwa hai duniani.

Tufanye nini kama taifa?

 1. Mabadiliko ya fikra. Kupata elimu au cheti sio kigezo pekee cha kuelimika
 2. Haki ya kupata elimu iwe ni haki ya kuelimika hasa katika kujikomboa kifikra
 3. Mfumo wa elimu uwe shirikishi na kuongozwa zaidi na wataalam na sio wanasiasa.
 4. Tuboreshe mfumo wetu wa kidemokrasia nchini, kwenye nyanja mbalimbali, sio kwenye siasa tu.
 5.  Tuhakikishe tunatumia tulichonacho kuwa na taifa lenye wananchi walioelimika.
 6. Tuwaunganishe wale wanaohesabika kuelimika kwa maslahi ya taifa. Idadi yao inahitajika kuwa kipeuo cha pili cha asilimia moja ya idadi ya Watanzania, kwa mfano kipeuo cha pili cha watu milioni 60 ni kadirio la watu 775
  Haya yatawezekana kwa urahisi iwapo tutaheshimu mawazo ya wananchi yaliyotolewa katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
  TANZANIA TUNAWEZA.