Aliyewahi kuwa Diwani wa kwanza na Mbunge wa kwanza kwa vyama vya upinzani mkoani Dar es salaam, Dokta Masumbuko Lamwai amefariki Dunia usiku wa kuamkia leo Mei, 05, 2020 jijini Dar es salaam.

Taarifa kutoka kwa ndugu wa familia zinasema kuwa Dkt Lamwai alipelekwa hospitali ya Rabininsia memorial iliyopo Tegeta jijini Dar es salaam jana usiku kabla ya madaktari kuthibitisha kifo chake mara tu alipofika hospitalini hapo.

Katika kipindi cha Uhai wake 1994, Dokta Lamwai aliwahi kuwa Diwani wa kata ya Manzese kupitia chama chetu cha NCCR-Mageuzi na kuweka rekodi ya kuwa diwani pekee na wa kwanza kutoka vyama vya upinzani Dar es salaam.

Mwaka 1995, Dokta Lamwai alijitosa kugombea Ubunge Jimbo la Ubungo kupitia chama chetu cha NCCR-Mageuzi na kufanikiwa kushinda na hivyo kuweka tena rekodi ya kuwa Mbunge pekee na wa kwanza kutoka vyama vya upinzani Dar es salaam.

Lakini pia Dokta Lamwai aliwahi kugombea Umeya wa Manisapaa ya Ubungo licha ya kushindwa kwenye uchaguzi ndani ya manispaa hiyo na baadaye kujivua uanachama ndani ya chama chetu na kujiunga na CCM mwaka 2000.

Aliwahi pia kuwa mbunge wa kuteuliwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipata nafasi hiyo kutoka kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu ndugu Benjamin William Mkapa.

Dokta Lamwai ambaye pia ni kaka wa Mbunge wa Jimbo la Rombo Ndugu Joseph Selasini ambaye hivi punde ametangaza kurejea NCCR-Mageuzi, alikuwa Mhadhiri Mwandamizi (Senior Lecturer) katika chuo kikuu cha Tumaini akifundisha masomo ya sheria.

Enzi za uhai wake akiwa ndani ya chama chetu cha NCCR-Mageuzi Dokta Lamwai alikuwa na wanasiasa wengine wakongwe kama vile Mabere Marando, Marehemu Dkt. Sengondo Mvungi, Augustine Mrema, Makongoro Nyerere, Prince Bagenda, Ndimara Tegambwe, Stephen Wassira na wengine wengi.

                                                                 

                             BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA, JINA LAKE LIHIMIDIWE. Amina